RAIS SAMIA: UTEKELEZAJI WA DIRA 2050 UNAHITAJI SEKTA BINAFSI IMARA NA YENYE UBUNIFU

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 unahitaji sekta binafsi yenye maarifa, ubunifu na uwezo wa kuzalisha bidhaa pamoja na kutoa huduma zinazoweza kushindana katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kuijenga na kuiwezesha kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.

"Nataka kuwahakikishia kwamba tutashirikiana kuijenga sekta binafsi yetu. Wafanyabiashara wa ndani wameanza kuvuka mipaka ya nchi na kuwekeza nje, lakini bado ni wachache. Tunataka kuwawezesha wengi zaidi kwa kuwatafutia fursa ili waweze kupanua biashara zao nje ya mipaka ya Tanzania," alisema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia alisema ndoto ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha uzalishaji, biashara na usafirishaji barani Afrika inaendelea kutimia hatua kwa hatua.

"Kwa muda mrefu tulikuwa tunasema Tanzania iwe kitovu cha biashara. Kadiri mambo yanavyoendelea, tunaelekea kufikia lengo hilo. Bado tuna kazi ya kufanya, lakini tayari tunaona mwanga wa mafanikio," alisisitiza.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam wakati Rais Samia akizungumza kuhusu maendeleo ya sekta binafsi na nafasi yake katika kufanikisha Dira ya Taifa 2050.


Comments