n Ngorongoro Wazindua Simulizi za Maajabu 7 - KU-Brand Tanzania!
n Olduvai na Mji
wa Rhapta Mhimili Mpya wa Uchumi;
n Tuzo za Wapiga
Picha/Tour Guides Ngorongoro Zaanza Rasmi;
n Spika Zungu,
Prof. Malebo Watia Neno.
Na Derek K. Murusuri, Ndutu, Ngorongoro
NDUTU, NGORONGORO 8 Februari, 2026 – DESTINATION NGORONGORO: Wakati habari za mji wa Tanzania uliozama majini karne ya pili (AD) kule Mafia, Ngorongoro inafichua maajabu 7 ya kusisimua kwa wakazi wa dunia, jambo linaloashiria mabadiliko makubwa kwenye vivutio vipya vya utalii na neema kubwa kwa uchumi wa Tanzania.
Uhifadhi na Utalii
wa Tanzania sasa unaingia katika kiwango cha juu nchini. Kamishna wa Uhifadhi
wa Mamlaka ya Uhifadhi la Eneo la Ngorongoro (NCAA), Abdul-Razaq Badru,
ameyataja maabu hayo katika uzinduzi rasmi wa kampeni kabambe ya "Simulizi
za Maajabu 7 ya Ngorongoro.”
Kamishna Abdul-Razaq Badru (katikati) akiwa pamoja na Manaibu Kamishna wake, katika uzinduzi wa kampeni ya Simulizi za Majaabu 7 ya Ngorongoro kupitia Kaulimbiu yao, Destination Ngorongoro, jana tarehe 7 Februari, 2026 huko Ndutu, Ngorongoro, mahali maalum ambapo nyumbu huenda kujifungua. Kushoto ni Naibu Kamishna Mariam Kobelo (Uhifadhi na Utalii) na kulia ni Naibu Kamishna Joas Mwakati (Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii). Kamishna Badru alipanda gari moja pamoja na waandishi wa habari katika safari ya kuelekea Ndutu.
Hatumaanishi
kuuacha utalii wa wanyama, la hasha, lakini mataifa yanayoingiza hela nyingi
sana duniani, si yale yanayofanya utalii wa wanyama, wakati umefika sasa, nasi
tunafanya mabadiliko makubwa kwenye vivutio vyetu ili kuvutia mamilioni ya
watalii duniani,” alisema
Mkakati wa
Diplomasia ya Utalii: Rhapta na Olduvai kama Muhimili Mpya wa Uchumi
Tanzania sasa
inapita kizingiti cha utalii wa asili na kuingia katika Utalii wa Kiurithi
na Akiolojia utakaobadilisha taswira ya nchi kimataifa. Huu ni mkakati wa
kuifanya Tanzania kuwa "Kitovu cha Kumbukumbu ya Dunia" kupitia mambo
makuu mawili:
Rhapta: Jiji Kuu
la Kwanza Afrika na Lango la Biashara ya Kale
Ugunduzi wa mabaki
ya mji wa kale wa Rhapta kule Kilwa—unaoaminika kuwa (Metropolis) jiji
kuu la kwanza ya Afrika iliyozama miaka 2,000 iliyopita—unaitambulisha
Tanzania kama kitovu cha biashara ya kimataifa tangu enzi za utawala wa Kirumi.
Kama alivyosisitiza Prof.
Hamis Malebo (UNESCO), huu ni utambulisho wa kipekee utakaovuta
wanasayansi, wanahistoria, na watalii wa anasa wanaotafuta simulizi za miji
iliyopotea.
Mabaki ya kuta za mji wa Rhapta, uliokuwa maarufu duniani katika miaka 2,000 iliyopita, uliozama katika bahari ya Hindi. Mji huu uliozama kwenye karne ya pili, unatarajiwa kufukuliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hiki ni kivutio kingine, pamoja Olduvai Gorge, ambalo ni chimbuko la binadamu, vitakwenda kuifanya Tanzania kupokea watalii kwa mamilioni. Katika mkakati mpya wa mabadiliko Ngorongoro (turn around strategy), vivutio vipya tofauti na vile vya asili vya wanyama vimeainishwa.
Olduvai Gorge:
Hija ya Binadamu na Utalii wa Jiolojia na Akiolojia: Tanzania
inashikilia hati miliki ya asili ya mwanadamu. Kupitia Olduvai Gorge, nchi
inatambulika kama "Nyumbani kwa Wote." Mhe. Musa Zungu ametoa
mwelekeo wa kimkakati wa kuanzisha Utalii wa Dini na Imani; ambapo Olduvai
inakuwa kituo cha hija ya kiakiolojia kwa kila binadamu duniani anayetaka
kuungana na asili yake.
Mapinduzi ya
Kiuchumi Yatokanayo na Utalii: Chini ya maono ya Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan, na kutafsiriwa na Kamishna Abdul-Razaq Badru, wa Ngorongoro, kuunganishwa
kwa "Mji uliopotea wa Rhapta" na "Chimbuko la Binadamu" Ngorongoro,
kunajenga bidhaa mpya ya kitalii (Niche Tourism).
Upekee wa
Kimataifa na Mkakati wa Brand Tanzania: Spika Musa Zungu hajakosea. Alikuwa
sahihi sana. Kamishna Badru alisisitiza katika retreat yao
iliyofanyika Dodoma wiki iliyopita kuwa, “Tanzania inakuwa nchi pekee
duniani inayotoa mchanganyiko wa The Big Five, Bahari ya Hindi, na Asili
ya Mwanadamu.”
Huu ni mwanzo wa
"Brand Tanzania" mpya; nchi ambayo si tu kituo cha mapumziko,
bali ni Maktaba Hai ya Historia ya Dunia.
Akizungumza jana (7Feb., 2026) katika viwanja vya Ndutu—eneo ambalo kwa sasa limepambwa na maelfu ya nyumbu wanaoshiriki katika msimu wa mazalia—Kamishna huyo ameweka bayana kuwa Ngorongoro si tu kivutio cha utalii, bali ni kitabu chenye kurasa saba za maajabu ambayo ulimwengu unapaswa kusoma na kuelewa.
“Mamlaka ya Ngongoro wako mbioni kukamilisha mkakati wa mabadiko ya taasisi (turn around strategy) unaokwenda kuleta mapinduzi makubwa katika shughuli za uhifadhi, utalii na jamii, ikiwa ni pamoja na utamaduni. “dunia yote itakuja kwao Ngorongoro, kwani ndio chimbuko la binadamu,” alisema Kamishna Badru.
Urithi wa Dunia na
Taji la UNESCO
Akianza simulizi hiyo tangu lango la Loduare, Kamishna Badru amesisitiza kuwa Ngorongoro ni sehemu ya Maajabu Saba ya Asili ya Afrika na inajulikana ulimwenguni kote kama "Ajabu la Nane la Dunia."
"Tanzania
tunajivunia kuwa na eneo pekee lenye Taji la Utatu la UNESCO (UNESCO Triple
Crown). Tunatambulika kwa urithi wa asili, thamani ya kiutamaduni, na umuhimu
wa kijiolojia. Hii inamaanisha Ngorongoro si mali ya Watanzania pekee, bali ni
hazina ya dunia nzima," alisema Kamishna Badru kwa msisitizo.
Kamishna Badru
akitoa maelezo ya binadamu wa kwanza walioishi katika bonde la Ngorongoro,
katika kituo cha UNESCO Global Geopark, Ngorongoro Lengai, jana.
Kivutio chenye
Maajabu Mengi: Ngorongoro haitambuliki kwa kivutio kimoja pekee. Ni eneo
lenye maajabu mengi— ya kiasili, kihistoria, kitamaduni, na kijiolojia— yote
yakiwa yameunganishwa ndani ya mandhari moja iliyohifadhiwa.
“Hapa, wanyamapori,
binadamu, sayansi, na utamaduni unaoishi vinashirikiana, hali inayofanya
Ngorongoro isiwe sehemu ya kutazama tu, bali sehemu ya kuelewa na kupata uzoefu
wa kipekee”, alisema Kamishna Badru.
Bonde la Kreta (Ngorongoro Crater): Kamishna Badru amelifananisha bonde hili na "Bustani ya Edeni." Ni kreta kubwa kuliko zote duniani ambayo haijamegeka, ikihifadhi maelfu ya wanyama katika uwiano wa kipekee.
Nyayo za Laetoli: Hapa ndipo simulizi ya mwanadamu inapoanza. Kamishna Badru amekumbusha kuwa zaidi ya miaka milioni 3.6 iliyopita, mwanadamu wa kwanza alipiga hatua zake hapa, akithibitisha kuwa Ngorongoro ni chimbuko la safari ya binadamu.
Pale Binadamu Wanapoishi Pamoja na Wanyama wa mwitu (Boma la Seneto): Kamishna Batu aliendelea kutoa simulizi iliyojaa elimu na hamasa, akifichua upekee wa Ngorongoro, ambapo jamii za Wamasai, Hadzabe, na Datoga zinaishi kwa amani na wanyamapori.
"Uhifadhi
hapa si tu kulinda ardhi, bali ni kulinda utambulisho na tamaduni zinazoishi,"
alisema.
Kamishna wa
Uhifadhi wa Mamlaka ya Eneo la Ngorongoro, Kamishna Abdul-Razaq Badru,
akimkabidha zawadi kiongozi wa Tour Guides nchini, Bw. Peter Mmbando,
ikiashiria kuzinduliwa kwa shindano la upigaji picha bora za video na mnato za
utalii, zinazihusu simulizi za maajabu ya Ngorongoro. Kulia ni Naibu Kamishna
Mariam Kobelo (Uhifadhi na Utalii), anayesimamia utalii katika Mamlaka hiyo.
Bonde la Olduvai – Chimbuko la
Binadamu: Bonde la Olduvai linasimulia hadithi ya kale zaidi kuliko
zote. Hapa ndipo vifaa vya kwanza kabisa vilipotengenezwa, na ambapo binadamu
alianza kufikiri, kukabiliana na mazingira, na kuanza safari yake.
Olduvai
inatukumbusha kuwa Ngorongoro si tu kivutio cha wanyamapori, bali ni Chimbuko
la Binadamu— mahali ambapo hadithi ya sisi sote ilianzia.
Ndutu: Muhimbili
ya Nyumbu, Nyumbu huja hapa kuzaa: Kila safari kuu ina
mwanzo wake. Huenda hapa ndipo kuna wakunga wa nyumbu wajawazito. Mbali na
maajabu ya Uhamaji huu wa Nyumbu (The
Great Wildebeest Migration), ujanja wao wote uko Ndutu.
Kila mwaka,
mamilioni ya wanyama hurejea katika nyanda hizi zenye rutuba kwa ajili ya
kuzaa. Ndani ya wiki chache tu, mamia ya maelfu ya ndama huzaliwa, wakihuisha
mfumo wa ikolojia na kuendeleza mojawapo ya harakati kuu za wanyamapori
duniani. Ndutu ndio nyumbani kwao.
Shindano la Picha za Utahifadhi na Utalii za Mnato na Video 2026: Wakati huo huo, katika kuwahamasisha Tour Guides nchini, pamoja na watengeneza maudhui nchini, Kamishna Abdul-Razaq Badru, amezindua shindano la kutengeneza maudhui ya utalii nchini.
Naibu Kamishna
Mariam Kobelo (kulia), anayeshughulikia uhifadhi na utalii, akiwa na kiongozi
wa Tour Guides Nchini, Bw. Peter Mmbando, baada ya uzinduzi wa shindano la
picha na video za ukuzaji wa sekta ya utalii katika hifadhi ya Ngorongoro jana
(7 Februari, 2026) huko Ndutu kwenya mazalia ya nyumbu.
Kamishna Badru
alitoa zawadi ya Bw. Ajabu, kwa kiongozi wa Tour Guides nchini, Bw. Peter
Mmbando, ikiashiria kuzinduliwa kwa shindano la upigaji picha bora za video na
mnato za utalii, zinazihusu simulizi za maajabu ya Ngorongoro. Hafla hiyo
ilihudhuriwa na Waandishi wa Habari, Wadau wa Utalii pamoja na baadhi ya
Watalii.
Maelezo ya
Hitimisho
Kamishna Badru
anaweka wazi, haya si maajabu yaliyotengana. Ni sura mbalimbali za hadithi moja
inayoishi. Kwa pamoja, zinaifanya Ngorongoro kuwa kivutio chenye maajabu mengi—
ya kiasili, kitamaduni, kihistoria, na yanayogusa maisha. Tanzania ina utajiri
mkubwa uliositiriwa, ambao sasa Ngorongoro wameanza hatua ya kuufukua
kivitendo. “Muda wa kuongea sana bila vitendo umepita. Sasa tunakwenda
kutumia potentials zote za utalii nchini kwetu ili taifa lipate neema Mwenyezi
Mungu aliyokusudia kwetu,” Kamishna Badru alihitimisha.
Derek K.
Murusuri ni mwandishi, mtafiti, na mshauri wa mawasiliano ya kimkakati,
biashara na mwandishi wa vitabu mwenye makazi yake jijini Dar es Salaam. Ni
mtaalamu wa miakakati ya mafanikio ya taasisi na kuandaa masimulizi yenye mvuto
wa kimataifa inayochochea ukuaji na mabadiliko ya kimkakati. Mfikie kupitia: derek.murusuri@yahoo.com

Comments
Post a Comment