Chama Cha Wananchi (CUF) kimeiomba Serikali kulichukulia kwa uzito mkubwa suala la utekaji, kupotea na kuawa kwa watu katika mazingira ya kutatanisha.
Rai
hiyo imetolewa leo Mei 29, 2025, jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa
Taifa wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, wakati akifungua mkutano
wa siku mbili wa Baraza la Uongozi la Taifa la CUF.
"Tupo
kwenye kikao hiki huku nchi yetu ikikabiliwa na majaribu makubwa. Kuna
malalamiko mengi kuhusu watu wanaodaiwa kutekwa, na hili ni suala zito
kwa taifa letu," alisema Prof. Lipumba.
Akaongeza:
“Hivi karibuni, Mchungaji Askofu Gwajima alisema ana orodha ya watu 83
waliopotea, baadhi yao wamepoteza maisha na wengine hawajulikani walipo.
Hili ni jambo kubwa sana kwa nchi yetu.”
Profesa
Lipumba alieleza kuwa suala la utekaji ndani ya CUF si jambo geni,
akitoa mfano wa tukio la mwaka 2017 ambapo Diwani wa Viti Maalum wa CUF,
Bi. Ziada Salum Nongwa, aliyekuwa akiishi Maporoni, Halmashauri ya
Kibiti, alikamatwa na watu wanaodhaniwa kuwa askari usiku akiwa na mtoto
wa mwezi mmoja, na hadi sasa hajulikani alipo
"Ziada
alikamatwa, akawekwa kwenye mtumbwi kuelekea visiwa vya Kibiti na tangu
siku hiyo hajawahi kuonekana. Mume wake alitufahamisha, nasi tukawa
sehemu ya jitihada za kumtafuta, hata barua iliandikwa kwa Waziri Mkuu,
lakini hadi leo hajapatikana," alisema.
Prof.
Lipumba alisema kuwa kitendo cha watu kupotea au kuchukuliwa bila
kufuata taratibu kinakiuka ibara ya 8, 14 na 15 za Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania zinazolinda haki za binadamu na ustawi wa wananchi.
Alisisitiza
kuwa kutokana na malalamiko haya, Serikali ina wajibu wa kutoa msimamo
na kuyachunguza kwa kina, huku akimhimiza Mchungaji Gwajima kuwasilisha
rasmi orodha na taarifa alizonazo kwa vyombo vya dola ili vifanye
uchunguzi huru na kutoa taarifa kwa umma.
Aidha,
Prof. Lipumba aligusia matukio ya watu waliokamatwa baada ya kufika
kusikiliza kesi ya Mheshimiwa Tundu Lissu na madai kwamba baadhi yao
walihusishwa na vitendo visivyofaa.
"Mimi
binafsi nimesikitishwa na kauli ya Mbunge wa Pandani, Bi. Mariam,
aliyoitoa bungeni kana kwamba anashabikia watu kuteswa na kuumizwa.
Tunapozungumzia haki sawa kwa wote, maana yake ni kwamba watu
wasifanyiwe matendo mabaya. Mbunge huyo alikuwa mdogo mwaka 2001, lakini
wakati huo visiwa vya Pemba vilipitia mateso makubwa," alisema.

Comments
Post a Comment