Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuimarisha mazingira bora na wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, hatua inayolenga kukuza uchumi wa Taifa kupitia sekta mbalimbali, hususan sekta ya utalii.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere (Sabasaba) jijini Dar es Salaam, Afisa Habari wa TAWA, Bw. Beatus Maganja, amesema taasisi hiyo inaendelea kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo utalii wa picha na uwindaji wa kitalii.
“Tunawaambia Watanzania na wawekezaji wote kwa ujumla kuwa TAWA ni mahali sahihi kwa uwekezaji, unapotaka kuwekeza unakaribishwa sana. Ikumbukwe kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa mazingira wezeshi Kwa wawekezaji wote wa ndani na nje ya nchi yetu ” alisema Maganja.
Kwa upande wake, Afisa Mhifadhi Mkuu kutoka TAWA, Dkt. Gladson Mlay, aliwahamasisha wananchi kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika maonesho hayo, ambapo wanaweza kujionea wanyamapori hai wakiwemo simba, chui, fisi, mamba na spishi mbalimbali za ndege.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwaalika wananchi kuonja na kununua kitoweo cha nyamapori choma kilichoandaliwa kwa umahiri, akisema kuwa ni njia mojawapo ya kuhamasisha matumizi ya rasilimali za maliasili kwa njia endelevu.
“Kwa wale ambao wanasema hawajawahi Kula nyamapori choma, nyama hiyo ipo hapa, mishikaki pia ipo na nyama ya kupeleka nyumbani nyumbani. Kwahiyo watu wote mnakaribishwa mje kuonja, Kula na kuona Kweli maliasili ni za kwetu wote” alisema Dkt. Mlay.

Comments
Post a Comment