TBN YAIPONGEZA SERIKALI, TCRA KWA KUWEZESHA MAFUNZO KWA WANABLOGU KUELEKEA UCHAGUZI 2025


Mtandao wa Wanablogu wa Tanzania (TBN) umetuma salamu za shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuona umuhimu wa kuandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanablogu katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.


Akizungumza katika mafunzo hayo ya siku moja yaliyofanyika leo katika ukumbi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, alisema juhudi hizo zinaonesha dhamira ya dhati ya Rais Samia kujenga taifa lenye amani, maendeleo na upatikanaji wa habari sahihi zenye uwajibikaji.

“Tunaishukuru Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Katibu Mkuu wake, ndugu Msigwa, kwa kutambua umuhimu wa TBN na kuwezesha mafunzo haya. Shukrani pia ziende kwa TCRA kwa kuandaa na kuratibu mafunzo haya muhimu,” alisema Msimbe.

Mafunzo hayo yalihusisha mada mbalimbali zikiwemo Mwongozo wa Waandishi wa Habari, Kanuni za Utangazaji wa Uchaguzi, maadili na sheria, na yalitolewa na wakufunzi kutoka tasnia ya habari akiwemo Dkt. Egbert Mkoko kutoka Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC).
Dkt. Mkoko aliwasisitiza wanablogu na waandishi wa habari kuzingatia uelewa wa wapiga kura, uwajibikaji kisiasa, kudumisha demokrasia na kuepuka kueneza uvumi au kushawishiwa na takrima.

Msimbe aliongeza kuwa blogu ni chanzo muhimu cha taarifa kwa jamii na hata kwa teknolojia ya akili mnemba (AI), hivyo ni lazima wanablogu waweke kipaumbele katika uandishi sahihi na wenye maadili. Alisisitiza kuwa AI ni nyenzo ya kusaidia na si mbadala wa ubunifu na hisia za kibinadamu.

“Tunahakikisha kuwa tutatumia majukwaa yetu kusambaza habari sahihi na za maendeleo, tukisaidia juhudi za serikali za kudumisha amani na mshikamano. Tunaamini mafunzo haya yatawawezesha wanablogu kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na uwajibikaji,” alisema Msimbe.

TBN, iliyoanzishwa rasmi Aprili 2, 2015, inawakutanisha wanablogu kutoka Tanzania na diaspora, ikiwa na lengo la kupanua uandishi wa habari za kidijitali zenye ubora na zinazozingatia maadili ya kitaifa.

Comments