MAKUNDI MBALIMBALI YA KIJAMII YAHIMIZWA KUILINDA AMANI: POLISI


Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeyataka makundi mbalimbali ya kijamii kudumisha na kuilinda amani ya nchi.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mbeya Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Apolinary Ndibahika Novemba 25, 2025 katika mkutano uliofanyika soko la SIDO Jijini Mbeya na kuhusisha Wafanyabiashara wa Mbeya Rice Group.

SSP Ndibahika amewataka wafanyabiashara hao kuhakikisha Amani na Utulivu vinaendelea kuenziwa, kulindwa na kudumishwa na kuwataka kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani kwani vitasababisha kukosa fursa ya kukuza uchumi wao kwa kufanya biashara.

Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Mbeya Mrakibu wa Polisi (SP) Nuru Mahenge ameyataka makundi hayo kujiepusha na matamshi na maneno mbalimbali ya uchochezi yanayotolewa na baadhi ya watu wasioitakia mema nchi yetu na kuwataka kujikita katika kazi za uzalishaji mali.

Naye, Mkuu wa Kituo cha Polisi Mwanjelwa Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Christina Kakiziba amewata Maafisa Usafirishaji (Bodaboda na Bajaji) kuacha kujihusisha na vitendo vya uhalifu kwani uhalifu haulipi na kamwe Jeshi la Polisi halitavumilia kuona vitendo hivyo, litachukua hatua kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mbeya Rice Group ndugu Abel Mwakipesile amewataka wafanyabiashara hao kushikamana, kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu, kuwafichua wahalifu pindi wanapoona watu wanaowatilia mashaka ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Comments