Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi Dkt.Moses Kusiluka,amewataka maafisa habari wa Serikali nchini kutambua wajibu wao wa kutoa taarifa sahihi kwa umma kuhusu kazi,mipango na mafanikio ya miradi ya Serikali.
Pia amewataka kukusanya kero za Wananchi na kuzifikisha kwa wakati kwa viongozi wa Serikali ili zipatiwe ufumbuzi kwa haraka iwezekanavyo.
Balozi Dkt.Kusiluka ametoa agizo hilo leo,Desemba 17, 2025, jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kikao Kazi cha Kitaifa cha Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais na Maafisa Habari wa Serikali, chenye kauli mbiu isemayo “Utu na Mawasiliano yenye Uwajibikaji”.
Balozi Dkt. Kusiluka amesema Serikali inawategemea wataalamu hao kama jeshi muhimu katika kutoa taarifa sahihi, kwa wakati na kwa ufasaha,hasa katika kipindi ambacho taarifa hasi na propaganda zinazoenezwa kupitia mitandao ya kijamii zenye nia ovu ya kuhatarisha usalama na mshikamano wa nchi.
Ameeleza kuwa kikao hicho kimeandaliwa kwa lengo la kuwaunganisha viongozi wapya na wataalamu wa habari mapema,kujenga uelewano wa pamoja,kubadilishana uzoefu na kuweka msingi imara wa ushirikiano katika kusukuma mbele ajenda za muhimu za Serikali.
Aidha,amebainisha kuwa maendeleo ya teknolojia ya habari yameleta fursa kubwa lakini pia changamoto,akionya kuwa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali yanaweza kuleta madhara endapo hayatadhibitiwa kwa weledi na uzalendo.
Sanjari na hayo,amewakumbusha Maafisa Habari kuwa wao ni watumishi wa umma walioajiriwa na wananchi, hivyo nafasi walizonazo ni dhamana inayopaswa kulindwa kwa kufanya kazi kwa bidii,uadilifu na kuzingatia maslahi mapana ya Taifa.
Balozi Dkt.Kusiluka ameongeza kuwa Serikali bado haijafanya vizuri katika kuwafikia wananchi kwa taarifa sahihi kuhusu miradi na mipango mikubwa ya maendeleo,hali inayosababisha wananchi kukosa uelewa wa fursa zilizopo na mchango wa Serikali katika kuboresha maisha yao.
Kutokana na hali hiyo,amewahimiza Maafisa Habari kujifunza kwa kina nyaraka muhimu za Taifa ikiwemo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025,mpango wa Dira ya Taifa ya 2050 pamoja na kujiendeleza kitaaluma kwa kutumia mbinu za kisasa za mawasiliano na kushirikiana na sekta binafsi.
Kwa upande wake,Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu,Bw.Bakari Machumu,amesema katika mazingira ya sasa yanayojaa changamoto na kasi ya maendeleo ya teknolojia, ni muhimu kwa Serikali kuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa za msingi kuhusu mafanikio na mwelekeo wa utekelezaji wa kazi zake,
Aidha Machumu amesisitiza kuwa kufanya hivyo husaidia kuelekeza mjadala wa umma,kupunguza upotoshaji wa taarifa na kuongeza uelewa na imani ya wananchi kwa Serikali.
Nae Mshauri wa rais masuala ya habari, Bw.Tiddo Muhando,amesema mawasiliano yanayozingatia ukweli,uwiano na uwakilishi wa maeneo yote ya nchi ni nyenzo muhimu katika kumsaidia Rais na Serikali kuelewa hali halisi ya wananchi na kuimarisha ufanisi wa mawasiliano ya Serikali kwa ujumla.Na: Mussa Agostiono wa @dunialeo, Dar es Salaam.

Comments
Post a Comment