Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Cuthbert Sendiga, leo Desemba 19, 2025 amezindua rasmi na kuhamasisha utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote (NHIF) katika Mkoa wa Manyara, akisisitiza umuhimu wa kila mwananchi kuwa na bima ya afya ili kupata huduma za matibabu kwa urahisi na kwa gharama nafuu.
Uzinduzi
huo umefanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT)
mjini Babati, na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, wataalamu wa afya,
wawakilishi wa mpango wa kitaifa wa Bima ya Afya kwa Wote pamoja na
wananchi mbalimbali.
Akizungumza
katika uzinduzi huo, Mhe. Sendiga amesema mpango wa Bima ya Afya kwa
Wote ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,
katika kutimiza ahadi ya siku 100 za kuanzisha mfumo utakaohakikisha
kila Mtanzania anakuwa na bima ya afya.
“Mfumo huu unalenga kumwondolea
mwananchi mzigo wa gharama kubwa za matibabu na kuhakikisha kila mmoja,
bila kujali kipato chake, anapata huduma bora za afya kwa wakati,”
amesema Mhe. Sendiga.
Aidha,
amewaelekeza Wasimamizi wa vituo vya kutolea huduma za afya mkoani
Manyara kuhakikisha mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unatekelezwa kwa
kuzingatia miongozo, kanuni na taratibu zilizowekwa, ili kufikia malengo
yaliyokusudiwa na Serikali.
Sambamba
na hilo, Mhe. Sendiga amesisitiza kuwa ni wajibu wa viongozi na
watendaji wote kwenda kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kujiunga na
mpango huo, ili waweze kunufaika na huduma za afya kwa uhakika.
Kwa
upande wake, Bi. Janeth Kibambo, Mwakilishi wa Timu ya Kitaifa ya
Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, amesema lengo kuu la mfumo huo ni
kuhakikisha wananchi wote wanakuwa na uwezo wa kupata huduma za afya
katika vituo vyote vya umma na binafsi vilivyosajiliwa, bila kikwazo cha
kifedha.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara,
Dkt. Andrew Method, ameeleza kuwa mkoa umejipanga kikamilifu kutekeleza
mpango huo, akibainisha kuwa changamoto ya wananchi kushindwa kugharamia
matibabu imekuwa kubwa, hivyo kuanzishwa kwa Bima ya Afya kwa Wote ni
mwarobaini muhimu katika kuboresha sekta ya afya.
Dkt.
Method ameongeza kuwa Mkoa wa Manyara uko tayari kuupokea na
kuutekeleza mpango huo kikamilifu, kwa kushirikiana na vituo vyote vya
afya na wadau mbalimbali, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora
na endelevu.
Uzinduzi
wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote mkoani Manyara unatarajiwa kuongeza
wigo wa upatikanaji huduma za afya, kupunguza vifo vinavyotokana na
ukosefu wa matibabu kwa wakati, na kuboresha ustawi wa jamii kwa ujumla.



Comments
Post a Comment