SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA

 


Serikali imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia sambamba na kuwezesha wanawake, vijana na makundi maalum, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kulinda haki za binadamu na kuimarisha ustawi wa jamii nchini.


Hayo yameelezwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake, Watoto na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Doroth Gwajima, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika Desemba 22, 2025, katika Kituo cha Ukombozi wa Kusini mwa Afrika jijini Dar es Salaam.

Amesema Serikali imeendelea kutekeleza kampeni mbalimbali za kijamii zinazolenga kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kukabiliana, kupinga na kutokomeza vitendo vya ukatili katika jamii, huku ikisisitiza mshikamano wa jamii kama nyenzo muhimu ya mafanikio ya mapambano hayo.

Dkt. Gwajima amebainisha kuwa Serikali, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Mashujaa wa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Ustawi wa Jamii, SmaUjataa Sauti ya Watoto Tanzania, CHAWATA, Malezi Bora Network pamoja na vikundi vya watu wenye ulemavu, imefanikiwa kuibua na kuimarisha vikundi vya kizalendo vinavyounga mkono juhudi za Serikali katika kufikia malengo ya ustawi wa jamii.


Amesema vikundi hivyo viliibuka kufuatia kuanzishwa kwa Wizara hiyo na vimeendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali katika kuibua, kukemea na kutoa elimu kwa jamii kuhusu vitendo vya ukatili, ambapo mafanikio yaliyopatikana yametokana na ushirikiano huo wa karibu.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, tangu kuanzishwa kwa kampeni hizo, jumla ya matukio 799 ya ukatili yameripotiwa na kushughulikiwa, huku Wizara ikiendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta mbalimbali, wakiwemo askari polisi 4,542, wasimamizi wa mashauri ya watoto wa kujitolea 15,255, wahudumu wa afya 10,534, maafisa ustawi wa jamii 1,342 pamoja na walimu wa unasihi na malezi 13,755.

Akizungumzia ushiriki wa wanawake katika uongozi, Dkt. Gwajima amesema kuwa kupitia Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2003, Serikali inaendelea kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha wanawake wanaongezeka katika nafasi za uongozi na maamuzi katika nyanja zote, ikiwemo kwa kushirikiana na vyama vya siasa.

Comments