Na Hawa Ismail- Dar es Salaam
TAASISI ya Utambulisho wa Bidhaa Tanzania (GS1 Tanzania) imeadhimisha miaka 15 tangu kuanzishwa kwake, mafanikio ambayo yameelezwa kuwa na mchango mkubwa katika kukuza biashara, viwanda na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Maadhimisho hayo yamefanyika leo Januari 24, 2026 jijini Dar es Salaam, yakihusisha wadau kutoka sekta binafsi, taasisi za umma pamoja na wataalamu wa teknolojia ya biashara.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa GS1 Tanzania, Fatma Kange, amesema taasisi hiyo imepitia safari ndefu ya mabadiliko tangu kuanzishwa kwake, kutoka utekelezaji wa shughuli za kimsingi hadi matumizi ya mifumo ya kisasa inayotumia teknolojia za kidijitali.
Amesema GS1 Tanzania inaendelea kubadilika kulingana na mahitaji ya soko na kasi ya mabadiliko ya teknolojia, huku maandalizi ya maadhimisho makubwa ya miaka 15 yakipangwa kufanyika rasmi Septemba mwaka huu.
“Kama taasisi tunajiuliza tulikotoka, tulipo na tunapoelekea. Teknolojia zinabadilika kwa kasi, na GS1 Tanzania ina wajibu wa kuhakikisha wanachama wake hawaachwi nyuma,” amesema Fatma.
Ameongeza kuwa mageuzi hayo yanalenga kuwawezesha wazalishaji na wafanyabiashara kutambulisha bidhaa zao kwa ufanisi zaidi na kwa viwango vinavyokubalika kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utafiti Viwanda wa TRIDO na Mwakilishi wa Mgeni Rasmi, Humfrey Ndosi, amesema GS1 Tanzania imekuwa chombo muhimu katika kusaidia viwanda vya ndani kuboresha ushindani wa bidhaa zao, hususan kwa kuwezesha matumizi ya mifumo ya utambulisho inayotambulika kimataifa.
Ameeleza kuwa kabla ya kuanzishwa kwa GS1, wazalishaji wengi walikumbana na changamoto kubwa za kuingiza bidhaa zao sokoni, hali iliyowalazimu baadhi yao kutegemea masoko ya nje.
Ndosi pia aliwasilisha salamu za wizara na kuipongeza GS1 Tanzania kwa mchango wake katika kukuza sekta binafsi, akibainisha kuwa serikali itaendelea kushirikiana na taasisi hiyo katika kujenga mazingira wezeshi ya biashara na kuimarisha miundombinu ya kiuchumi.
Amesema mafanikio ya GS1 Tanzania yametokana na ushirikiano mpana kati ya serikali na sekta binafsi, ukihusisha taasisi mbalimbali zikiwemo TRIDO, TBS, BRELA, SIDO, TPSF, ZNCC, TCCIA, CTI, TAHA pamoja na vyama vya wazalishaji wa mazao na viungo.
Katika maadhimisho hayo, GS1 Tanzania imetangaza kuendeleza zaidi mageuzi ya kidijitali, yakiwemo maandalizi ya uzinduzi wa mfumo wa 2D Migration, unaolenga kuboresha utambulisho wa bidhaa za Tanzania na kuongeza ufanisi katika minyororo ya thamani ya biashara.
Ufunguzi wa maadhimisho hayo umetumika kutoa wito kwa Watanzania kujiamini, kujituma na kutumia fursa zilizopo katika mazingira bora ya biashara yanayoendelea kuwekwa na serikali

Comments
Post a Comment