TAASISI 300 KUUNGANISHWA MFUMO MPYA ‘IDRAS’ WA MAPATO WA TRA

 

Na Hawa Ismail- Dar es Salaam 

Jumla ya taasisi 300 zinatarajiwa kuunganishwa na mfumo mpya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) unaojulikana kama IDRAS, hatua inayolenga kuboresha usimamizi wa kodi za ndani na kupanua wigo wa kodi nchini.

Akizungumza leo Januari 21, 2026 jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Alfred Mregi, amewataka wafanyabiashara  wa ndani kutumia mfumo wa IDRAS, akieleza kuwa ni mfumo wa kisasa unaosimamia kodi za ndani na kuwahusisha watumishi wa TRA pamoja na wadau wa nje.

Mregi amesema kupitia mfumo huo, TRA itaweza kupanua wigo wa kodi kwa kusajili wafanyabiashara wapya pamoja na kurahisisha utekelezaji wa majukumu yake.


 Amefafanua kuwa awamu ya kwanza itahusisha kuunganisha kampuni 60 kati ya taasisi 300 zinazotarajiwa kuingia kwenye mfumo huo, hatua itakayowezesha TRA kupata taarifa pana na sahihi.

“Kwasasa tunahakikisha shughuli zetu nyingi zinafanyika kupitia mfumo. Hatua hii itarahisisha kila kitu, kupunguza muda kwa wafanyabiashara na kuwaondolea adha walizokuwa wakizipata wakati wa kulipa kodi. Mfumo huu ni rafiki kwa mtumiaji na unachakata taarifa kwa haraka,” amesema Mregi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wafanyabiashara Mkoa wa Dar es Salaam, Pendo Lucas, amesema mafunzo yaliyotolewa kuhusu matumizi ya mfumo wa IDRAS yamewapa wafanyabiashara imani kubwa kuwa utaondoa changamoto na malalamiko yaliyokuwepo hapo awali. Amewahimiza wafanyabiashara wote kuupokea mfumo huo na kuendelea kuiunga mkono TRA.


Aidha, Lucas amesema kwa sasa hakuna mgogoro kati ya wafanyabiashara na TRA, akisisitiza kuwa huduma zinatolewa kwa karibu bila ubaguzi. “Tumekuwa marafiki, na sasa tunapokutana nao tunawafuata kwa kujiamini,” amesema.

Naye Mhasibu Mkuu wa Kampuni ya Yongda International Energy Trading Co. Limited, Benny Birigileki, amesema mfumo wa IDRAS umejibu maswali mengi ya walipa kodi na utawezesha ulipaji wa kodi kwa urahisi zaidi kwa kuondoa vishoka na kuongeza uwazi katika mifumo ya kikodi.


Comments