TUME YA TEHAMA KUCHOCHEA MABADILIKO YA KIDIJITALI KUELEKEA DIRA YA TAIFA 2050

Na Noel Rukanuga, Dar es Salaam

Serikali imesisitiza kuwa maendeleo ya Taifa kuelekea Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2050 hayawezi kufikiwa bila uwekezaji madhubuti katika rasilimali watu wa TEHAMA, sera rafiki za kidijitali na mazingira wezeshi kwa ubunifu wa kiteknolojia.

Akifungua Kongamano la Tisa la TEHAMA (TAIC 2026) leo Januari 19, 2026 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, amesema Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICTC) ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha wataalamu wa TEHAMA wanasajiliwa, kuendelezwa na kulindwa kitaaluma ili kuchochea maendeleo ya sekta hiyo.

Mhe. Kairuki amebainisha kuwa pamoja na kukuza wataalamu, Serikali inalenga kuona kampuni changa bunifu (startups) zinapata mifumo madhubuti ya usimamizi na msaada wa kitaalamu ili bidhaa na huduma zao ziweze kushindana sokoni na kuchangia ukuaji wa uchumi wa kidijitali.


“Ni muhimu taasisi zote za umma na binafsi kutoa taarifa za mifumo yao ya TEHAMA na kuonyesha namna inavyounganishwa na mifumo mingine. Aidha, wabunifu wanapaswa kutumia teknolojia mpya kama Akili Unde kwa kuzingatia maadili na misingi ya Taifa letu,” amesema.

Katika kuimarisha ujumuishi, Waziri huyo amepongeza waandaaji wa kongamano hilo kwa kutenga siku maalum kwa ajili ya Wanawake katika TEHAMA, akieleza kuwa hatua hiyo inaendana na azma ya Serikali ya kuhakikisha wanawake na wasichana wanashiriki kikamilifu katika mapinduzi ya kidijitali.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga, amesema kongamano hilo ni jukwaa muhimu la kitaifa linalowawezesha wadau kujadili kwa kina nafasi ya mapinduzi ya kidijitali katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Dkt. Mwasaga amesema kwa kipindi cha siku tano, wataalamu wa ndani na nje ya nchi, sekta ya umma na binafsi pamoja na makampuni ya teknolojia wanapata fursa ya kubadilishana uzoefu na kupendekeza mikakati itakayoharakisha maendeleo ya kidijitali nchini.

Kongamano la TAIC 2026 linaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Mabadiliko ya kidijitali yanayochochea athari za kijamii na uvumbuzi wa kiteknolojia kwa Taifa lenye mafanikio, haki, ujumuishi na kujitegemea.”

Kaulimbiu hiyo inaakisi dhamira ya Taifa ya kutumia teknolojia kama nyenzo ya kuimarisha usawa wa kijamii, kukuza ubunifu na kujenga uchumi unaojitegemea kuelekea mwaka 2050.




Comments