SERIKALI imetangaza neema ya kihistoria kwa wanablogu, vijana wabunifu, na watoa maudhui mtandaoni nchini kwa kupunguza ada za leseni kwa kiwango kikubwa, hatua inayolenga kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali na kurasimisha shughuli za wahabarishaji wa mitandao
Hatua
hiyo imekuja kufuatia utafiti wa kina na mikutano ya kimkakati ya
takribani mwaka mzima kati ya mtandao wa Tanzania Bloggers Network (TBN)
na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ikielezea vikwazo vya
gharama vilivyokuwa vikikwaza uandishi wa habari za kidijitali nchini.
Akizungumza
katika ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Watoa Huduma za Utangazaji (ABC
2026) jijini Dodoma leo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Mhe. Hamisi Mwinjuma, amesema ada ya leseni kwa watoa maudhui
mtandaoni imeshushwa kutoka Sh500,000 hadi Sh50,000 tu, huku ada ya
maombi ikiwa ni Sh10,000 pekee.
Mageuzi
hayo pia yamegusa kundi la wakusanyaji wa maudhui (Online Content
Aggregators), ambao ada yao imeshushwa kutoka Sh1,000,000 hadi Sh100,000
pekee. Aidha, kundi la "Amateteur" limeanzishwa kwa ajili ya vijana
wanaochipukia ili waweze kujitambulisha rasmi na kukuza vipaji vyao bila
vikwazo vya kifedha.
Mapinduzi ya Teknolojia ya DSB
Wakati
neema hiyo ikitangazwa, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Bakari,
ametangaza kuanza kwa teknolojia mpya ya utangazaji wa redio ya
kidijitali nchini inayojulikana kama Digital Sound Broadcasting (DSB).
Teknolojia
hiyo itaanza kufanya kazi katika mikoa mitano ya majaribio ya Dar es
Salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha, na Mbeya, lengo likiwa ni kuongeza ubora
wa sauti na huduma za utangazaji nchini.
"Tumekamilisha
maandalizi yote ya kiudhibiti na watoa huduma wa miundombinu
wameshapatikana. Hii ni hatua kubwa ya kuendana na mabadiliko ya
teknolojia duniani na kuimarisha utangazaji, hususan maeneo ya
vijijini," alisema Dkt. Bakari.
Utafiti: Redio Bado ni Kinara
Katika
mkutano huo, Injinia Andrew Kisaka wa TCRA amewasilisha matokeo ya
utafiti wa hali ya utangazaji kwa mwaka 2025/2026, ukionyesha kuwa redio
inaendelea kuwa chanzo kikuu cha habari kwa asilimia 85 ya Watanzania.
Hata
hivyo, utafiti huo umebaini ukuaji mkubwa wa matumizi ya intaneti
miongoni mwa vijana, ambapo asilimia 45 hupata habari kupitia mitandao
ya kijamii kabla ya kusikiliza redio au kutazama televisheni.
Upande
wa televisheni, utafiti unaonyesha asilimia 65 ya watazamaji wanatumia
ving'amuzi, huku maudhui ya ndani yakipendwa zaidi kwa asilimia 70.
Serikali imewahimiza watoa huduma za kienyeji kuwekeza zaidi kwenye
majukwaa ya kidijitali (OTT) ili kukidhi mahitaji ya soko la sasa.
Ulinzi wa Hakimiliki na Mikopo
Ili
kuhakikisha wanahabari wa kidijitali wanufaika na kazi zao, Serikali
imezielekeza taasisi za COSOTA na TCRA kuandaa mpango wa kulinda
hakimiliki na kudhibiti uharamia mtandaoni. Aidha, Serikali imeanza
kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa watengeneza maudhui kwa ajili ya
ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi.
Hadi
kufikia Desemba 2025, TCRA imetoa jumla ya leseni 707 za utangazaji,
zikiwemo 318 za maudhui mtandaoni, jambo linaloashiria kukua kwa uhuru
wa habari na demokrasia nchini chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu
Hassan.

Comments
Post a Comment