Na WAF, Dodoma
Serikali imesisitiza kuwa huduma za afya kwa akina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano zinaendelea kutolewa bure kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, na kwamba vitendo vya kutoza gharama kwa makundi hayo haviruhusiwi.Hayo yameelezwa leo Februari 3, 2026 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, wakati akijibu swali la Mhe. Bakari Bakari Shingo (Ukonga), aliyeuliza iwapo Serikali ina mpango wa kukemea vitendo vya kutoza gharama za matibabu kwa wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Ameongeza kuwa Serikali imeshatangaza rasmi kuanza utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (UHI) awamu ya kwanza, itakayohusisha makundi maalum ya wananchi yakiwemo watoto, wajawazito, watu wenye ulemavu na wazee wasio na uwezo, ambapo gharama za bima kwa makundi hayo zitagharamiwa na Serikali.
Dkt. Samizi amesema kukamilika kwa hatua hiyo kutawezesha wazee wasio na uwezo pamoja na makundi mengine yaliyoainishwa kupata huduma za afya kwa kugharamiwa na Serikali, hivyo kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote.

Comments
Post a Comment