Na Hawa Ismail, Dar es Salaam
Wananchi wametakiwa kubadili mtazamo kuhusu taka na kuziona kama fursa ya kiuchumi badala ya uchafu, kufuatia juhudi zinazoendelea za kutoa elimu ya usimamizi sahihi wa taka zinazoongozwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Hatua hiyo ni sehemu ya maandalizi ya kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Taka Sifuri yanayotarajiwa kufanyika Machi 30 mwaka huu, ambapo maonesho maalum yanaendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria NEMC, Hamad Kissiwa, amesema lengo ni kuongeza uelewa wa jamii kuhusu thamani ya taka katika uchumi na mazingira, akisisitiza kuwa taka zinaweza kurejelewa na kutumika kama malighafi ya bidhaa mbalimbali.
Amesema kupitia elimu hiyo, wananchi wanaoneshwa namna taka zinavyoweza kuzalisha bidhaa kama nguo, mbolea, chakula cha mifugo pamoja na kuchangia upatikanaji wa madini kupitia urejelezaji wa taka za kielektroniki.
Kissiwa ameongeza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanabeba kaulimbiu inayolenga kuangazia tatizo la upotevu wa chakula, akibainisha kuwa taka za chakula ni chanzo kikubwa cha uzalishaji wa gesi chafuzi zinazochangia mabadiliko ya tabianchi.
Amesema tafiti zinaonesha kuwa kati ya asilimia 8 hadi 10 ya taka za chakula zinazopelekwa dampo huzalisha gesi hatarishi, hivyo kuna umuhimu wa jamii kubadili tabia ya matumizi na uhifadhi wa chakula.
Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki maonesho hayo ili kujifunza na kunufaika na fursa zilizopo katika sekta ya usimamizi wa taka.
Katika maonesho hayo, wadau mbalimbali wameonesha ubunifu wa kutengeneza bidhaa zenye thamani ya kiuchumi kutoka kwenye taka, hatua inayochochea ajira na kuongeza kipato kwa wananchi.
Kwa upande wake, Afisa Rasilimali Watu wa Kampuni ya Chilambo General Trade Company Limited, Maria Michael, amesema kampuni hiyo inajihusisha na ukusanyaji, usafirishaji na utunzaji wa taka hatarishi ikiwemo za kielektroniki, kemikali, mafuta machafu na mabaki ya dawa.
Amesema taka hizo huchakatwa katika viwanda maalum kwa kutenganishwa kulingana na aina zake ili kurahisisha urejelezaji, ambapo vifaa kama chuma, bati na sehemu za mashine hutolewa kwa uangalifu kabla ya kupelekwa kwa wataalamu.
Ameongeza kuwa kampuni hiyo pia hutoa elimu kwa jamii kuhusu usimamizi sahihi wa taka hatarishi ili kulinda afya za wananchi na mazingira kwa ujumla.

Comments
Post a Comment