Na: Hawa Ismail
Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi cha Mahakama Kuu ya Tanzania, Zahra Maruma, amesisitiza umuhimu wa kuongeza ushiriki wa wanawake katika utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala (ADR), akieleza kuwa hatua hiyo itaongeza ubora, usawa na ufanisi katika utoaji wa haki nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Machi 27, 2026 wakati wa kongamano la kitaifa la mawakili wakati alipomwakilisha Wakili Mkuu wa Serikali Dkt.Ally Possi ambapo alisema lengo la kongamano hilo lililenga kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika sekta hiyo, amesema Tanzania inalenga kuwa kitovu cha ubora wa usuluhishi barani Afrika na duniani.
Amebainisha kuwa kuboreshwa kwa mifumo ya kisheria na sera kutatoa fursa zaidi kwa jamii kutumia usuluhishi kama njia mbadala ya kutatua migogoro, hali itakayochangia kujenga amani na utulivu kwa mujibu wa dira ya maendeleo ya taifa.
Aidha, ameongeza kuwa serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mkazo katika kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa wakati, kwa gharama nafuu na kwa usawa kwa wananchi wote.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Usuluhishi Tanzania (TIAC), Godson Nyange, amesema matumizi ya ADR husaidia kutatua migogoro kwa haraka na kwa gharama nafuu, hivyo kuwawezesha wananchi na wafanyabiashara kuendelea na shughuli za uzalishaji.
Amesema hatua hiyo pia inachochea ukuaji wa uchumi kwa kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha imani ya wawekezaji nchini.
Naye Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Leticia Petro, amesema bado kuna pengo kubwa la ushiriki wa wanawake katika sekta hiyo, akitaja takwimu zinazoonyesha kuwa wanawake ni asilimia 28 pekee huku wanaume wakiwa asilimia 72 katika shughuli za usuluhishi, upatanishi na uamuzi wa migogoro.
Ameeleza kuwa kongamano la siku tatu limeandaliwa ili kutoa elimu, hamasa na uzoefu kwa wanawake wanaojihusisha na usuluhishi, pamoja na kuwahamasisha mawakili vijana kuona nafasi yao na umuhimu wao katika jamii.
Hata hivyo, amebainisha kuwa changamoto hizo zinatokana na mitazamo ya kijamii, ukosefu wa fursa za mafunzo pamoja na mifumo dhaifu ya kuwaendeleza kitaaluma, na kutoa wito kwa wadau kushirikiana kuweka mazingira wezeshi ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta hiyo muhimu.

Comments
Post a Comment