Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la SUMA JKT, Brigedia Jenerali Shija Lupi, amesema Shule ya Sekondari Jitegemee ni miongoni mwa shule kongwe zinazojivunia kuibua vipaji mbalimbali vinavyowasaidia wanafunzi kujitegemea maishani.
Amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa mahafali ya shule hiyo, akiwahimiza wanafunzi kuongeza juhudi katika masomo yao ili kufikia malengo waliyojiwekea na kuchangia maendeleo ya taifa.
Aidha, Brigedia Lupi ameeleza kuwa kuna mipango ya kuikarabati na kuiboresha shule hiyo kwa kujenga miundombinu ya kisasa itakayokidhi mahitaji ya sasa ya elimu.
Amesema miongoni mwa maboresho hayo ni ujenzi wa jengo la ghorofa nne litakalojumuisha ofisi, maabara na madarasa, hatua itakayoiwezesha shule hiyo kuwa ya kisasa zaidi.
" Shule ya Sekondari Jitegemee inaendelea kuwa chachu ya kuibua vipaji, hususan katika michezo, akitolea mfano wa mchezaji Goma Lugema anayewakilisha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 na kufanya vizuri" amesema Brigedia Lupi
Pia amebainisha kuwa mbali na masomo ya darasani, shule hiyo inawajengea wanafunzi nidhamu pamoja na ujuzi wa ujasiriamali, ikiwemo utengenezaji wa sabuni za matumizi mbalimbali, jambo linalowawezesha kujitegemea kiuchumi wakiwa bado masomoni.
Shule ya Sekondari Jitegemee imeadhimisha mahafali yake ya 32 ya kidato cha sita, ikiwa ni taasisi inayotoa elimu kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita. Kwa mwaka 2026, jumla ya wahitimu 80 wamehitimu, wakiwemo wasichana 28 na wavulana 52.

Comments
Post a Comment