Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo amesema serikali inaendelea kuboresha mifumo ya upatikanaji wa pembejeo ili kuhakikisha zinawafikia wakulima kwa wakati na kwa gharama nafuu, hatua inayolenga kuongeza tija hasa katika zao la pamba.
Ameeleza kuwa maboresho hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha sekta ya kilimo ili iweze kuchangia kwa kiwango kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Chongolo ametoa kauli hiyo Aprili 16, jijini Dodoma, wakati wa mkutano wa wadau wa tasnia ya pamba uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, ukiwa na kaulimbiu isemayo “Nguvu ya pamoja kwa Tasnia ya Pamba Endelevu.”
Aidha, amesema Sera ya Kilimo ya mwaka 2023 inaelekeza kila kijiji kuwa na afisa ugani mmoja, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya serikali ya kuinua uchumi wa mkulima ifikapo mwaka 2030.
Amebainisha kuwa wakulima wengi wa pamba bado wanatumia mbinu duni za uzalishaji, hali inayosababisha kushuka kwa tija licha ya baadhi yao kumiliki mashamba makubwa.
Kutokana na changamoto hiyo, serikali imejipanga kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza uzalishaji na ufanisi katika kilimo cha pamba.
Sambamba na hilo, serikali inaendelea kuwekeza zaidi katika sekta ya kilimo kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa pamba, kuinua kipato cha wakulima na kukuza uchumi wa wananchi kwa ujumla.
Chongolo amesisitiza kuwa mkutano huo ni jukwaa muhimu la kujadili mikakati madhubuti ya kuendeleza tasnia ya pamba, ambayo ni miongoni mwa mazao muhimu ya biashara nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameishukuru Bodi ya Pamba kwa kuchagua mkoa huo kuwa mwenyeji wa mkutano huo, akiahidi kuwa mkoa utaendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuimarisha sekta ya kilimo.

Comments
Post a Comment