Na: Florah Nkondola
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) imesema imepata faida ya shilingi bilioni 22.9 mwaka uliopita, huku ikitarajiwa kupata faida tena mwaka huu,hali inayochangia kuwa shirika hilo lina himarika kifedha baada ya miaka mingi ya changamoto.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania, David Nchimbi, wakati wa uzinduzi wa kituo kipya cha TTCL cha Experience Centre kilichopo Kijitonyama, Dar es Salaam, kinacholenga kuwaonyesha Watanzania jinsi ya kutumia huduma za intaneti kwa ufanisi zaidi majumbani na maofisini.
Nchimbi amebainisha kuwa lengo la TTCL ni kuwaunganisha Watanzania wenyewe kwa wenyewe na pia na dunia, kupitia miundombinu ikiwemo Mkongo wa Taifa unaotumika na makampuni yote ya mawasiliano nchini, akisisitiza kuwa kupata faida kumekuwa sehemu ya utamaduni wa kampuni hiyo na kuongeza kuwa kituo hicho kitaonyesha namna intaneti inavyoweza kutumika kwa njia mbalimbali majumbani, ikiwemo kudhibiti taa, mfumo wa usalama, kamera za nyumbani, pamoja na kufurahia muziki katika vyumba mbalimbali bila kukatizika, huku akisisitiza kuwa TTCL inataka Watanzania wafike nyumbani na kuweka simu pembeni.
Aidha amekiri kuwa huduma kwa wateja bado inahitaji kuboreshwa, akiahidi kuwa kabla ya mwisho wa mwaka huu maboresho makubwa yatakuwa yamefanyika, na kusema atakuwa tayari kukutana na waandishi wa habari kutoa taarifa ya hatua zilizofikiwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, amesema kuwa mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka 10 wenye malengo matatu muhimu, ikiwemo kujikita zaidi kuwahudumia wateja, kupanua matumizi ya teknolojia ya kisasa na kuongeza aina za bidhaa na huduma zinazotolewa.
Aidha amekanusha madai yaliyoenezwa baada ya taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kutolewa, akisema baadhi ya watu walijaribu kudanganya umma kwamba TTCL ilitengeneza hasara ya shilingi bilioni 7, hali ambayo amesema si kweli kabisa kwani kampuni ilipata faida ya bilioni 22.9.
Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa huduma ya FTX inayowakilishwa katika kituo hicho inalenga kutoa intaneti ya fiber majumbani, maofisini na maeneo ya wazi kama viwanja vya mpira, stendi za SGR, vivukoni, masoko mbalimbali pamoja na vyuo, hali inayoonesha upanuzi mkubwa wa huduma za TTCL nchini.

Comments
Post a Comment