Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Shukrani Kyando, amewakumbusha wananchi wote wanaomiliki ardhi kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi ya ardhi (land rent), akisisitiza kuwa umiliki wa ardhi unaambatana na wajibu wa kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Aprili 24, 2026, Kyando amesema kila Mtanzania ana haki ya kumiliki ardhi, lakini ni lazima alipe kodi ya ardhi kwa mujibu wa sheria.
Amesisitiza kuwa ulipaji huo si hiari bali ni wajibu unaopaswa kutekelezwa na kila mmiliki wa ardhi.
Kyando amebainisha kuwa katika mkoa wa Dar es Salaam, kupitia wilaya zote tano, wamebaini takribani wananchi 600 wenye madeni makubwa ya kodi ya ardhi. Amesema idadi hiyo ilipatikana baada ya kufanya uchambuzi kwa kuchukua sampuli ya wananchi 100 kutoka kila wilaya.
Ameeleza kuwa tayari ofisi yake ilitoa notisi kwa wadaiwa zaidi ya miezi mitatu iliyopita, ikiwa ni pamoja na kuwafikia moja kwa moja katika maeneo yao na kuwapa elimu pamoja na kuwataka kulipa madeni yao. Hata hivyo, amesema bado kuna baadhi ya wananchi hawajatekeleza wajibu huo.
"Serikali imetoa muda wa nyongeza wa wiki mbili kwa wadaiwa kulipa kodi ya ardhi kabla ya kuchukua hatua za kisheria, ikiwemo kuwafikisha mahakamani, huku akisisitiza kuwa taratibu zote za busara zinafuatwa kabla ya hatua hiyo" amesema Kyando
Kwa upande wake, Mratibu wa Kodi Mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Liapa, amesema wameendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulipa kodi ya ardhi kupitia njia mbalimbali, ikiwemo vipindi vya televisheni, redio, kliniki za ardhi, matangazo ya magari mitaani na ujumbe mfupi wa simu.
Aidha, Kyando ameongeza kuwa kutolipa kodi ya ardhi kunasababisha madhara mbalimbali, ikiwemo kushindwa kuitumia ardhi kama dhamana, kutozwa riba ya adhabu ya asilimia moja, pamoja na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Comments
Post a Comment