VIJANA 100 BORA WACHAGULIWA KUENDELEA NA SHINDANO LA VIJANA UCHUMI CHALLENGE 2026

 


Na Hawa Ismail- Dodoma 

Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya Vijana Uchumi Challenge, Amina Sanga, ametangaza rasmi majina ya washiriki 100 bora waliofanikiwa kuingia hatua inayofuata ya Shindano la Vijana Uchumi Challenge 2026 baada ya mchakato wa ushindani mkubwa ulioshirikisha maombi 7,852 kutoka mikoa yote ya Tanzania.

Amesema shindano hilo lenye kaulimbiu isemayo “Wanafikiri, Taifa Linasonga” linalenga kuibua mawazo bunifu ya vijana yatakayosaidia kuimarisha uchumi wa Tanzania dhidi ya athari za misukosuko ya kiuchumi duniani, sambamba na kutekeleza maono ya Serikali ya Awamu ya Sita na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


Sanga amesema mwitikio wa vijana ulikuwa mkubwa ambapo sekta ya TEHAMA na huduma za kidigitali iliongoza kwa asilimia 30.7 ya mawazo yaliyowasilishwa, ikifuatiwa na kilimo na teknolojia za kilimo kwa asilimia 27.8, huku sekta ya viwanda na uzalishaji ikichangia asilimia 21.3 ya mawazo yote yaliyopokelewa.

Ameeleza kuwa baada ya uchambuzi wa awali, maombi 4,121 sawa na asilimia 52.5 yalitimiza vigezo vya msingi vya shindano, na kati ya hayo mawazo 458 yalipata alama za juu na kufikishwa katika hatua ya mwisho ya tathmini kabla ya kupatikana washiriki 100 bora waliotangazwa.

Kwa mujibu wa Sanga, washiriki hao wamechaguliwa kutokana na ubora wa mawazo yao, kiwango cha ubunifu, uwezo wa mawazo hayo kutekelezeka pamoja na mchango wake katika kukuza uchumi wa Taifa.


 Ameongeza kuwa kufika katika hatua hiyo ni mafanikio makubwa kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo.

Aidha, washiriki 100 bora wataingia katika kambi maalum ya mafunzo kwa siku nne ambapo watapatiwa mafunzo ya kitaalamu na ushauri wa kuboresha mawazo yao kabla ya kufanya mawasilisho yatakayowezesha kupatikana washiriki 30 bora wa nusu fainali na baadaye washiriki 10 bora watakaoingia hatua ya fainali.

Sanga amesema kutokana na mwitikio mkubwa na ubora wa mawazo yaliyowasilishwa, zawadi za shindano zimeongezwa ambapo mshindi wa kwanza atapata shilingi milioni 50, mshindi wa pili milioni 30 na mshindi wa tatu milioni 20. Washiriki wote 100 bora watapatiwa vyeti vya utambuzi pamoja na fursa za mafunzo, ushauri wa kitaalamu na kuunganishwa na wadau mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza mawazo yao kwa manufaa ya Taifa.

Comments