Vijana wanaotoka katika jamii zinazoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro wanatarajiwa kunufaika na fursa zaidi za elimu ya juu baada ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kuzindua mwongozo wa utekelezaji wa Ngorongoro Scholarship Fund.
Mpango huo unalenga kuwawezesha vijana kupata elimu ya juu na kuzalisha wataalamu watakaotoa mchango katika uhifadhi wa maliasili, utalii, maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, alisema mpango utaanza kutekelezwa katika mwaka wa masomo wa 2026/2027 kwa wanafunzi waliopata udahili katika vyuo vikuu nchini.
Alisema katika awamu ya kwanza, wanafunzi 15 watanufaika na ufadhili huo baada ya NCAA kutenga shilingi milioni 99 kwa ajili ya kugharamia masomo yao.
Dkt. Kiwia alieleza kuwa kipaumbele kitatolewa kwa wanafunzi watakaosomea taaluma zinazochangia uhifadhi na maendeleo ya eneo la Ngorongoro, ikiwemo uhifadhi wa maliasili na mazingira, usimamizi wa wanyamapori, uhifadhi wa malikale na utalii.
Aidha, alisema maombi ya ufadhili huo yataanza kupokelewa kuanzia Agosti 15, 2026 kupitia mfumo wa kidijitali wa HESLB, huku akiwaomba waombaji na walezi kuzingatia vigezo vilivyowekwa katika mwongozo wa mfuko huo.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Bi. Gloria Bideberi, alisema kuanzishwa kwa Ngorongoro Scholarship Fund ni sehemu ya juhudi za mamlaka hiyo kuwekeza katika elimu na kuboresha maisha ya jamii zinazoizunguka Hifadhi ya Ngorongoro.
Alibainisha kuwa NCAA imekuwa ikitoa ufadhili wa masomo kwa zaidi ya miaka 30 katika fani mbalimbali, zikiwemo ualimu, udaktari, uhandisi, uhasibu na uhifadhi, hatua iliyosaidia kuongeza wataalamu katika jamii na taifa.
Bi. Bideberi alisema kupitia ushirikiano huo, HESLB itasimamia utoaji na ufuatiliaji wa ufadhili, huku NCAA ikiendelea kutenga fedha kila mwaka ili kuhakikisha mfuko huo unakuwa endelevu na kuwafikia wanafunzi wengi zaidi.
Pia aliwahimiza taasisi za umma, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na washirika wa maendeleo kuunga mkono mfuko huo, akisisitiza kuwa ni uwekezaji muhimu katika elimu, uhifadhi wa maliasili na maendeleo ya jamii.
Comments
Post a Comment