VIJANA WATAKIWA KUSOMA MAMBO NJE YA 'BOX' NA KUJENGA MAADILI: SHEIKH JALALA


Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu Shia Ithna'ashariyyah Tanzania (TIC), Hemed Jalala, amewataka vijana nchini kujenga utamaduni wa kutafiti na kujifunza mambo mapana zaidi ya yale wanayoyafahamu, akisisitiza kuwa maarifa ni msingi muhimu wa kukabiliana na changamoto za kizazi cha sasa.

Jalala amesema hayo wakati wa Matembezi ya Amani ya kumbukizi ya kifo cha Mtume Muhammad (s.w.w.w) yaliyofanyika Dar es Salaam, akieleza kuwa vijana ndio kundi linalokumbwa na changamoto nyingi na hivyo linahitaji kuelekezwa katika maarifa, maadili na akhlaq.

Amesema vijana wanapaswa “kusoma mambo nje ya boxi”, kufanya tafiti na kuzama katika masuala mbalimbali badala ya kuyachukulia mambo juu juu.

Kwa mujibu wa Sheikh Jalala, vijana pia wanapaswa kuzingatia maadili na akhlaq, akisema kumbukizi ya maisha na kifo cha Mtume Muhammad (s.w.w.w) inapaswa kuwa chachu ya vijana kujenga tabia njema na mwenendo unaofaa katika jamii.

Aidha, amewataka vijana kutambua nafasi yao katika maendeleo ya taifa na kuepuka kuwa chanzo cha migogoro na vurugu.

“Vijana ndio chachu ya maendeleo ya nchi, kwa hiyo wasiwe sababu ya kuvuruga nchi yao; wawe sababu ya kuitengeneza njia,” amesema Sheikh Jalala

Comments