Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu Baraka Leonard, amesema Bunge la Tanzania lipo tayari kujifunza na kushirikishana uzoefu na mabunge mengine duniani ili kuboresha utendaji wa shughuli za kibunge.
Baraka ameyasema hayo Oktoba 7, 2026, wakati akitoa hotuba katika Mkutano wa Makatibu wa Bunge wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) unaofanyika jijini Arusha, sambamba na Mkutano wa 153 wa IPU katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).
Amesema hakuna Bunge linaloweza kudai kuwa linajua kila kitu, hivyo ushirikiano na kubadilishana uzoefu kati ya mabunge ni muhimu katika kuboresha mifumo na taratibu za kibunge.
“Tunatambua kuwa hakuna Bunge linalojua kila kitu, mbinu yetu ni kujifunza kutoka kwa wengine na kushirikishana uzoefu,” amesema.
Akizungumzia mifumo mbalimbali ya kibunge, Baraka amesema tofauti zilizopo kati ya mabunge duniani ndizo zinazoufanya Umoja wa Makatibu wa Bunge kuwa muhimu katika kujifunza na kubadilishana uzoefu.
Amesema baadhi ya nchi zina mfumo wa mabunge mawili, huku Tanzania ikiwa na Bunge moja, na kwamba lengo la mikutano hiyo si kuamua mfumo gani ni bora, bali kuelewa mifumo mbalimbali na kujifunza yale yanayofanya kazi katika mazingira tofauti.
“Tunakutana si kupanga ni mfumo gani bora zaidi, bali kuelewa ni nini kinachofanya kazi, kwa nini kinafanya kazi na ni mafunzo gani tunaweza kuyachukua,” amesema.
Baraka amesema Umoja wa Makatibu wa Bunge unatoa fursa ya kujifunza kuhusu taratibu za kibunge, namna taasisi zinavyohifadhi mwendelezo wa shughuli zake, kuwasaidia Wabunge, kukabiliana na mabadiliko na kudumisha ufanisi katika mazingira yanayobadilika kwa kasi.
Aidha, amesema Bunge la Tanzania linaendelea kukabiliana na mabadiliko ya haraka, yakiwemo mabadiliko ya matarajio ya wananchi, maendeleo ya teknolojia na ongezeko la mahitaji ya uwazi katika shughuli za Bunge.
Amesema Bunge limeingia katika mfumo wa kidijitali kupitia Bunge Mtandao (e-Parliament), unaowawezesha Wabunge kupata nyaraka kwa njia ya mtandao na kutekeleza majukumu yao bila kutegemea nyaraka za karatasi.
Vilevile, amesema Bunge limeongeza upatikanaji wa shughuli zake kwa umma kupitia Televisheni ya Bunge na mitandao ya kijamii, hatua inayowawezesha wananchi kufuatilia shughuli za Bunge moja kwa moja.
Katika hotuba yake, Baraka amewakaribisha washiriki wa mkutano huo jijini Arusha, akisema timu yake imeandaa mazingira yatakayowezesha wadau hao kubadilishana uzoefu, kujifunza na kushirikiana kitaalamu.
Amesema Arusha kwa muda mrefu imekuwa ikihusishwa na diplomasia, majadiliano, ushirikiano wa kikanda na ushiriki wa kimataifa, hivyo kufanyika kwa mkutano huo jijini humo kuna umuhimu katika kuimarisha ushirikiano wa taasisi za kibunge duniani.
Comments
Post a Comment