KWAGILWA: FURSA ZA UCHUMI WA BLUU ZIWAFIKIE WAFANYABIASHARA NA WAWEKEZAJI

 

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Reuben Kwagilwa, amesema ukanda wa Bahari ya Hindi una fursa nyingi za biashara na uwekezaji ambazo zinapaswa kutumiwa kikamilifu na wafanyabiashara, wajasiriamali na wawekezaji.

Kwagilwa ameyasema hayo leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, wakati akizungumza katika Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12).

Amesema mkutano huo umezikutanisha nchi wanachama wa ukanda wa Bahari ya Hindi kwa lengo la kujadili fursa mbalimbali za kibiashara na uwekezaji zinazopatikana katika ukanda huo, ikiwemo Tanzania.

Kwa mujibu wa Kwagilwa, moja ya maeneo yenye fursa kubwa ni uchumi wa bluu, unaojumuisha shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazofanyika baharini, maziwa na mito.

Ametaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni kilimo cha mwani, ufugaji, usafirishaji wa mizigo kupitia bandari, utalii, michezo ya baharini, uvuvi, uchimbaji wa madini pamoja na utafutaji wa nishati baharini.

Amesema shughuli hizo kwa ujumla zinaunda mnyororo mpana wa uchumi wa bluu ambao unaweza kutoa fursa kubwa za biashara, ajira na uwekezaji kwa wananchi.

Kwagilwa amesema jukwaa hilo limewakutanisha wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wajasiriamali, taasisi za kifedha na benki, taasisi za utafiti, vyuo vya elimu ya juu pamoja na wavumbuzi, kwa lengo la kujadili namna bora ya kutumia fursa hizo.

Amesema lengo kuu ni kuhakikisha wadau hao wanatoka na maazimio ya pamoja yatakayosaidia kuendeleza matumizi endelevu ya fursa zinazopatikana katika uchumi wa bluu wa ukanda wa Bahari ya Hindi.

Comments